The Extent You Know The Truth, The Extent You will Enjoy Salvation

Monday, October 3, 2011

Kumbukumbu Haiozi....Waponyeni Watu...Part 1

WAPONYENI WATU.
Rescue the perishing.
Part [A]
Tenzi 60 Nyimbo Standard NS 88.
Na, Frances Jane Fanny Crosby 1820- 1915
 
 
Frances Jane Fanny Crosby [almaarufu km Fanny] alizaliwa mnamo March 24, 1820 huko South East, New York na aliitwa kuanza maisha mapya mbinguni yapata February 12, 1915 huko Bridgeport, Connecticut. Ameishi duniani kwa kipindi cha miaka 94, miezi 10 na siku 19. Fanny alimweleza mama yake kuwa, “kama wakati wa kuzaliwa ningepewa kuchagua, bado ningechagua kubaki kipofu… kwa sababu nitakapokufa uso wa kwanza nitakaokutana nao ni ule wa mbarikiwa Mwokozi wangu.” 
Kipofu kwa maisha yake yote yaliyofuata, Fanny Crosby, mwandishi maarufu wa nyimbo za MUNGU katika historia ya Kanisa la Kristo, baadaye aliandika, "Na nitamwona uso kwa uso, na kusimulia kuwa nimeokolewa kwa neema." Ingawa kipofu, alishuhudia zaidi ya mashairi yake  8,000 yakiingizwa kwenye muziki na zaidi ya nakala 100,000,000 za nyimbo zake zikichapishwa. Takriban watu 200 waliotumia majina ya kiuandishi [pen names] akiwamo Grace J. Frances, walipewa kazi zake na wachapishaji wa vitabu vya nyimbo za MUNGU hivyo umma usingejuwa aliandika kiasi kikubwa cha nyimbo hizo. Aliweza kuandika mashairi yapatayo saba kwa siku.
Mara kadhaa aliposikia wimbo mgeni ukiimbwa, alitafuta kujuwa mtunzi wake ni nani na kuishia kugundua kuwa wimbo ni wake yeye mwenyewe!   Akiwa amezaliwa kwenye familia iliyokuwa ikiishi katika banda tu, baba yake aliyeitwa John hakuwezakukumbukwa na Fanny kwa kuwa alifariki dunia Fanny akiwa na umri wa miezi 12 tu duniani. Wakati Fanny akiwa na wiki sita tu za kuzaliwa, alipata shambulio la homa ya macho.
Tabibu wa familia hakuwepo kipindi hicho. Badala yake tabibu mwingine aliitwa kuja kumtibia. Alimwandikia atumie dawa ambayo ni mafuta ya moto ya haradali itumike machoni, ambayo iliua kabisa uonaji wa macho yake! Ilikuja kugundulika baadaye kuwa yule tabibu hakupata mafunzo ya kazi ya utabibu, lakini walichelewa kumshitaki baada ya kugundua kuwa alitoroka mji na hakusikika tena. Fanny wala hakujutia kamwe masaibu yale na wala hakumhesabia hatia yule tabibu kishoka, bali aliamini hali ile iliruhusiwa na Bwana kukamilisha mpango wake kwa maisha yake.
Kama kawaida ya huruma na uchungu wa mama kwa mtoto, mama yake Fanny alijiweka kwenye mzani na kujikuta ni mjane na isitoshe katoto kake hako kamoja tena kanakuwa kipofu, mama huyu kwa kutumia hekima zake alikuwa tayari kufia maisha ya binti yake huyu, ilimradi tu amwandae kwa maisha ya furaha licha ya ulemavu huu mkubwa wa kutisha. Akiwa na umri wa miaka 5 alichukuliwa na mama yake kupelekwa kwa mtaalamu wa macho aliyebobea ambaye aliheshimika nchini, Dkt. Valentine Mott.
Majirani na marafiki wakafanya changizo la pesa kwa ajili ya kumpeleka kupata matibabu. Jibu la kutisha lilitoka kinywani kwa yule mtaalam, "Masikini mtoto, ninasikitika hutawezakuona tena maisha yako yote." Fanny hakuwaza kama alikuwa wa kuhurumiwa kiasi hicho. Siyo kupoteza kuona ndiyo kulisumbua moyo wake wa ujana bali ni wazo la kuwa hatoweza kupata elimu kama wavulana na wasichana wengine. Kwa mshangao, katika umri wa miaka 8, alichapisha shairi lake la kwanza: “Ooh nii moyo gani wa furaha kiasi hiki! Ingawa siwezi kuona, nimeamua kuwa katika dunia hii, nitakuwa wa kuridhika. Ni baraka ngapi nafurahia, ambazo watu wengine hawana. Kulia na kuomboleza kwa sababu ni kipofu siwezi na sitowahi!”
Fanny alikuwa wa umri wa miaka 9 familia ilipohamia Ridgefield, Connecticut, ambapo aliishi mpaka umri wa miaka 15. Mama alikuwa mkarimu na aliyetingwa na shughuli kwa ajili ya kuishi kwao wawili, kwa hiyo alikuwa ni nyanya yake ambaye hakujakusahaulika katika maisha yake. Nyanya yake alitumia muda mwingi kumuelezea vitu vya asili ya dunia na mbinguni. Pia alimtambulisha Fanny kwenye Biblia na kitabu hiki cha MUNGU kikajakuwa maarufu kwake kuliko kingine kiwacho chote. Alianza kurarua neno. Inasadikika katika rika la utoto aliwezakuweka kwenye kumbukumbu zake vitabu 5 vya Musa [the Pentateuch], vitabu vya Ruthu, Zaburi kadhaa, kitabu cha Mithali, Wimbo ulio bora, na sehemu kubwa tu ya Agano Jipya! Hii ilimjengea dhana, matamanio, na uwezo wa kuwasilisha ujumbe kwa ajili ya nyimbo zake za injili zisizochuja.        
Mashairi 2 maarufu sana ya vipofu wawili wa kihistoria, Homer na Milton, ziliunganishwa na nyingine mahiri za Fanny Crosby, ambaye alichapisha shairi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 11 tu.  Karibia na kumbukumbu yake ya kuzaliwa ya miaka 15, lilikuja tangazo la furaha kwamba mama yake angewezakumpeleka shule mpya, taasisi ya vipofu iliyoko jijini New York. Fanny alipiga makofi kwa furaha na kulia, "Ooh ashukuriwe MUNGU, amejibu maombi yangu, kama ambavyo nilijuwa atafanya." Ilikuwa ni mwezi March 3, 1835, kwamba Fanny alipanda gari moshi kuelekea Norwalk na baadaye boti mpaka New York City. Alitumia miaka mingine 23 iliyofuata ya maisha yake pale, kama mwanafunzi kwa miaka 12, na badaye kama mwalimu kwa miaka 11 zaidi. Tangu utotoni mwake binti kipofu alisikia mwito ndani yake wa kuandika ushairi, na beti fupi kadhaa zilikuja toka kinywani mwake. Shuleni uwezo wa akili zake ulianzakujielezea wenyewe kwa nguvu mpya. William Cullen Bryant alizuru shule siku moja na kumtia moyo sana,
baada ya kupata fursa ya kusoma beti zake. Fanny alisema baadaye kuwa “mgeni huyu hakujuwa ni mangapi ametenda kwa maneno yake hayo machache ya kumtia moyo” Siku nyingine, Dr. Combe wa Boston alichunguza vichwa vya wanafunzi vipofu. Kama alivyohisi kichwa chake, alisema:
hapa kuna mshairi mwanamke. Mtieni moyo kadri inavyowezekana. Msomeeni vitabu vizuri na mfundisheni mazuri yaliyo kwenye ushairi. Mtakuja kusikia siku moja huko juu ya huyu binti.
Mashairi yalianza kutawala ndani ya moyo wake na akili yake. Katika majira ya kipupwe cha mwaka wa 1843, alipokuwa na umri wa miaka 23, alikuwa mgeni kipofu katika baraza la Congress Marekani. Alitoa heshima zake kwa baraza hilo kwa staili ya shairi lake na baadaye akatoa heshima kwa Bwana kwa staili hiyo hiyo. Alitoa hotuba isiyo ya kujichanganya wala simulizi ya kutisha bali alitema mashairi kuhusu upendo wa agape wa Mwokozi. Aliongea kwa ushawishi, kama vile ameonana uso kwa uso na Mwokozi.
Baraza la Congress alilolihutubu lilihudhuriwa na marais wastaafu, wanasiasa maarufu na ma-seneta wa Marekani kama: John Quincy Adams, Thomas E. Benton, Hamilton Fish, Henry A. Wise, Alexander Stevens, Jefferson Davis, and Robert Toombs. Akilihutubia baraza hili, machozi yalionekana yakishuka kwenye shavu za baadhi ya waheshimiwa hawa, kwa maana haijalishi udogo wala ukubwa wa mtu, maelfu elfu walipokea ujumbe wake kama mafuta ya uponyaji kwa ajili ya Roho. Kama matokeo ya ushuhuda wake, alianza kuwa na marafiki ambao ni wanasiasa na viongozi wa dini wazito maarufu wa nyakati zake na hakuna aliyeweza kumsahau mara walipokutana naye.
Katika maisha yake alipata kuwafahamu marais wote isipokuwa George Washington. Rais wa nane wa Marekani Van Buren aliyetawala kipindi cha 1837–1841 aliwahi kula naye dina na kufanyika kuwa mmoja wa marafiki wake wakubwa. Alitoa ujumbe wa kinabii kuhusu ubora wa William Henry Harrison aliyekuja kuwa rais wa tisa wa Marekani aliyetawala kwa siku 32 tu na kufa kwa homa ya mapafu [Pneumonia] ni rais asiyejulikana na wengi. Wakati rais John Tyler alipozuru taasisi ya vipofu, Fanny alimkaribisha kwa shairi jipya kama ilivyokuwa kawaida yake ajapo mgeni basi anapakuwa tungo jipya la kumkaribisha na hivyo kupendeka kwa watu maarufu kwa kuwa aliwapa tungo kila mmoja kwa heshima yake na kubaki kama kumbukumbu ya mgeni huyo.
Urafiki wake na rais wa 11 James Knox Polk ulikuwa wa karibu sana na wa kutamanisha, rais huyu ambaye pamoja na rais wa 7 Andrew Jackson walifanyika wanaharakati wa kupinga biashara ya utumwa [kupinga watu kuteswa]. Alifaidi urafiki wa karibu sana na rais Grover Cleveland aliyekuwa rais kwa vipindi viwili tofauti, rais wa 22 na 24 (1885–1889 na 1893–1897) kwa zaidi ya nusu karne, kwa sababu pia aliwahikuwa katibu wa taasisi ya vipofu wakati huo pia akifundisha. Alijijengea nidhamu isiyo ya kawaida katika maisha yake na ya kazi na mara nyingi alitingwa na kunakili mashairi yake.
Wageni wengi walifika shuleni kwao na kutengeneza kumbukumbu za maisha yao yote. Pindi alipokuja Jenny Lind aliimba na Fanny Crosby alikariri shairi lake lililoitwa "The Swedish Nightingale." Wakati Henry Clay alipozuru shule yao, binti Crosby aliteuliwa kutunga shairi kwa heshima yake. Alipomaliza, Clay alimtwaa mikononi mwake na kusema, "Hili silo shairi pekee ambalo ninawiwa kwa huyu binti. Miezi 6 iliyopita alinitumia baadhi ya mistari kufuatia kifo cha mpendwa kijana wangu. Kijana Clay aliuwawa vitani Mexico. Wakiwa wamesimama pamoja kiongozi huyu mkubwa wa kitaifa na mwanatenzi huyu kipofu walimwaga machozi. Akingali shuleni, kitabu chake cha kwanza kuchapishwa akiwa na umri wa miaka 24 kilipewa kichwa “The Blind Girl and Other Poems/Binti Kipofu na Mashairi Mengine”. Pia alighani nyimbo kadhaa maarufu na kusaidia kuandika kile kilichokujakuitwa Kantate ya kwanza [first cantata] iliyochapishwa Marekani.
Katika umri wa miaka 27, alifanyika mkufunzi shuleni, nafasi aliyoshikilia hadi 1858, alipoondoka shuleni. Pamoja na udhihirisho wote wa kuzama katika Kristo ambao tayari aliushirikisha katika namna nyingi, ilikuwa vigumu sana kuamini kuwa alikuwa hajaokoka mpaka 1851, umri wa miaka 31. Huu mwanzo wa utukufu ulitukia katika huduma ya uamsho uliofanyika huko Old John Street Methodist Church jijini New York ambapo alijiunga. Akitafakari tukio miaka ya baadaye, alisema: “Baada ya maombi kufanyika, walianza kuimba tenzi maarufu ya zamani ya kuwekea watu wakfu nchini kwao uliojulikana kama `Alas! And Did My Saviour Bleed?/masikitiko mwokozi wangu alimwaga damu' na walipofika mstari wa 4 wa ubeti wa 5 usemao `Here, Lord, I give myself away/Hapa Bwana naisalimisha nafsi yangu' moyo wangu ulifurikwa na nuru ya nje.
Mahaba [Romance] pia yalidhihirika katika maisha ya Fanny Crosby. Mapema katika umri wa miaka ipatayo 20, alijiingiza katika mahusiano na kijana kipofu aliyeitwa Alexander VanAlstyne. Alikuwa mpenzi wa muziki na alitekwa na mashairi ya Fanny. Pia binti Fanny alivutiwa na utamu uliomtesa wa muziki wa kijana Alex. Baadaye, Alex aliandika baadhi ya tenzi za Fanny na kuoana  kwa miaka ipatayo 44. Siku moja katika mwezi wa June Alex alimwimbia kipenzi chake wimbo wa moyo wake. Fanny anasimulia: Kuanzia saa hiyo nafsi mbili zikaendea ulimwengu mpya, kwa kuwa upendo ulikutana na upendo mwenzake na hivyo dunia nzima ikabadilishwa. “Kamwe hatukuwa tena vipofu, kwa maana nuru ya upendo ilinyesha pale mti wa waridi ulipostawi katika mazingira ambapo maji meupe yaliyofunikwa na mimea iliyochanua kwa staili ya mkeka na kufunika maji ambayo yalishuka toka kwenye mwamba wa chemichemi.”
Alex naye alikuwa mwalimu na kwa zaidi ya miaka 15 urafiki wao ulistawi. Mwisho, mnamo  Machi 5, 1858, Fanny aliolewa katika umri wa miaka 37. Maisha yalikuwa ndiyo yanaanza kwa Fanny Crosby, kwa maana maisha ya huduma yake yalikuwa yakingali mbele. Maisha ya ndoa yalikuwa ya furaha sana na VanAlstyne, ambaye aliishi hadi 1902. Ndoa hii ilipata mtoto mmoja aliyetwaliwa na mauti akingali mchanga. Labda tukio hili lilimsaidia Fanny kughani, Salama mikononi mwa Yesu, ambao ulifariji maelfu elfu ya wazazi waliopata huzuni za tukio kama la kwake la kufiwa mtoto. Katika ndoa yake alipania kutumia jina: mama VanAlstyne lakini mumewe alisisitiza kuwa aendelee kutumia jina la mzazi wake ambalo tayari lilijulikana sana. Baadaye wanandoa hawa walikuja kujiunga na kanisa la Methodist la barabara ya kumi na tatu jijini New York. Fanny Crosby alibaki kuwa muumini wa kimethodist maisha yake yote. Kupitia  Peter Stryker, mtumishi wa Kanisa la mabadiliko la kidachi jijini New York, Fanny alikutana na mwimbaji maarufu William Bradbury. Alimpa Fanny makaribisho mwororo: Fanny, namshukuru MUNGU kwamba hatimaye tumekutana, kwa maana nafikiri unaweza kuandika nyimbo za MUNGU, na nimetafuta siku nyingi kukutana nawe kwa maongezi. William alipendekeza kwamba Fanny ajaribu kuja na tungo japo moja kwa ajili yake juma lile. Huu ulikuwa ni mwanya ambao Fanny aliutamani na kuungoja. Ndani ya siku 3 tu alirudi na kuwasilisha wimbo wake wa kwanza wa utukufu, ubeti wa awali ulisomeka: Twaenda, twaenda kwenye mji ng’ambo ya anga, ambapo maeneo ni mazuri, na nuru ya jua haifi kamwe.
Hii ilikuwa ni mwaka wa 1864, Fanny akiwa na umri wa miaka 44. Sasa mustakabali wake ulianza na huu ulikuwa wimbo wake wa kwanza uliotumika shule ya jumapili. Simulizi zingine za mashairi yake maarufu zilifuata: Pass Me Not ulikuwa wimbo wake wa kwanza kuitamalaki dunia kwa umaarufu. Akifanyia kazi pendekezo la rafiki yake, William H. Doane, Fanny alighani wimbo huu mwaka 1868 baada ya kuhudumu gerezani. Alipokuwa akiongea na wafungwa, mmoja alilipuka kwa kilio, "O Bwana, usinipite!" Aliguswa sana na kwenda nyumbani na kughani tungo lake maarufu. Ira Sankey alisema, "Hakuna utenzi uliokuwa maarufu sana kwenye mikutano ya injili London mwaka 1875 kama huu." Mlevi mmoja wa ki-england alisikia kusanyiko likiuimba na kujisemesha mwenyewe taratibu, "Oh, natamani asingenipita." Usiku uliofuata huduma ilianza na wimbo huo na yule mlevi aliokolewa. Alianza kubeba nakala ya ule wimbo kila siku na miaka 40 baadaye akiwa kama mfanyabiashara maarufu Marekani, alikutana na Fanny na kumpa dola 20.
Safe in the Arms of Jesus/salama mikononi mwa Yesu ulichukuliwa na baadhi ya watu kama wimbo wake maarufu. Siku moja, katika mwaka wa 1868, Doane alifika na kusema, "Dada Fanny, nina dakika chache kabla ya treni ninayostahili kupanda haijaondoka kuelekea Cincinnati lakini kwanza, utaweza kunifanyia upendeleo kabla sijapanda hiyo treni? Nahitaji wimbo mpya kabisa ambao ninawezakuutambulisha kwa mara ya kwanza kabisa katika mkutano; wimbo ambao utagusa nyoyo na fikra za vijana na watoto. Panaenda kuwepo mkutano mkubwa wa shule ya jumapili katika jimbo zima huko Cincinnati mwezi ujao na, ikiwa ni pamoja na ujumbe mkubwa wa watu wazima, vijana wengi na watoto wanategemewa kuhudhuria. Tunahitaji sana huu wimbo mpya." Akiwa tayari na tuni/vocal kichwani, Fanny alisema “Sikiliza kwa makini,” na akageukia piano, akakaa chini na kuanza kupiga tuni yake hiyo mpya kwa namna ya kutamanisha na kuamsha hisia. Fanny alisema, "Muziki wako unasema, `Safe in the Arms of Jesus/Salama mikononi mwa Yesu." Akiiendea meza yake, alitwaa kipande cha karatasi, akapata kalamu, akaketi chini, na kuanza kuandika. Akiwa anapiga, aliendelea kuandika. Alikunja karatasi ile na kuitia ndani ya bahasha, na kuikabidhi kwa rafiki yake. Kwa sabau treni ilikuwa inaondoka ndani ya dakika 35 tu, alisema “kaisome ndani ya treni na fanya hima, kwa kuwa hutaki kuchelewa!" Ndani ya treni alisoma maneno ambayo baadaye Sankey aliyafanya maarufu, na mioyo ilikujakuyaimba toka nyakati hizo. Simulizi zilizo katika wimbo huu zinashangaza sana, alisema Sankey. Fanny akiwa anamsindikiza Doane kupanda teksi, mara dereva wa teksi akafikiri kuwa abiria wake alikuwa Fanny Crosby na siyo Doane, dereva wa teksi alivua kofia yake na kulia machozi. Walipofika stesheni ya treni dereva teksi alimwita askari polisi kikosi cha reli na kumweleza amwongoze mtumishi Fanny salama kwenda kwenye treni na kuongeza kuwa, "Tuliimba Safe in the Arms of Jesus/Salama mikononi mwa Yesu kwenye msiba wa binti yangu mdogo juma lililopita."
Wakati Askofu James Hannington alipouawa kinyama na majambazi huko Uganda, Afrika, shajala [diary] yake iligunduliwa. Ndani yake alieleza alivyoburuzwa kwenda kuuawa wakati huo akiimba Safe in the Arms of Jesus/Salama mikononi mwa Yesu. Alikuwa hata akicheka katikati ya machungu yake yale.
Simulizi la kushangaza linasimuliwa kuhusiana na vita katika mwaka wa 1918. Mhandisi wa Kifini [A Finnish engineer] anasimulia alivyozungusha mji na kuteka idadi fulani ya wafungwa weupe. 7 kati yao walikuwa wapigwe risasi alfajiri ya jumatatu iliyofuata. Mmoja wa wahanga alianza kuimba wimbo huu unaopendeka sana, Safe in the Arms of Jesus/Salama mikononi mwa Yesu, ambao ndiyo alitoka kujifunza majuma 3 tu yaliyopita kutoka Jeshi la Wokovu [Salvation Army]. Mmoja baada ya mwingine wa wale marafiki 7 wahanga alikwenda magotini na kuanza kuomba. Waliomba waruhusiwe kufa bila kuzibwa nyuso zao huku mikono yao ikiinuliwa kuelekea Mbinguni, waliimba wimbo huu walipoelekezwa kwenda kwenye machinjio yao ambako walikuwa waanze maisha mengine ya uzima wa milele nje ya dunia hii. Mhandisi huyu wa Kifini, Nordenberg, ambaye alikuwa afisa wa zamani wa jeshi, aliyeleta simulizi hili, mwenyewe alikutana na Kristo katika muda ule ule wa chinjachinja ile kama matokeo ya ushuhuda wake wa tukio lile.
Waponyeni Watu/Rescue the Perishing Tenzi No. 60, uliandikwa mwezi Julai kipindi cha joto katika mwaka wa 1869. Katika misheni, Fanny alikuwa akihubiri kusanyiko kubwa la watu, katika mojawapo ya sehemu mbaya sana za jiji la New York, the Bowery. Wakati akihudumu alihisi kufurahishwa kuwa kijana fulani yatima wa mama lazima aokolewe usiku ule. Alitoa tamko la wokovu na kijana wa miaka 18 alijihudhurisha mbele ya madhabahu na kupaza sauti, "Niliahidi kukutana na mama yangu Mbinguni lakini niishivyo hivi sasa, hiyo itakuwa haiwezekani." Fanny aliomba pamoja na hii Roho ya thamani [precious soul] na aliokoka kwa shangwe yule kijana. Aliinuka toka magotini kwake, akiwa na nuru mpya machoni pake, na kusema, "Sasa naweza kukutana na mama yangu Mbinguni, kwa kuwa nimempata MUNGU wake!"
Rafiki mmoja alitoa maoni, "Siyo kwamba ni ajabu sana mambo ambayo ziara hizi za ukombozi zinafanya?" Akiwa amepanda farasi wa kukodi na akiwa kati ya Bowery na Brooklyn, Fanny alianza kuandika akingali juu ya farasi akihofia kwamba hana muda wa kutosha kusubiri mpaka afike nyumbani. Katika chumba chake alikamilisha mistari ya wimbo kabla kuchoka. Asubuhi iliyofuata, maneno yalitolewa vivuli/copy, liriki/lyrics zake zilinukuliwa na kutumiwa kwa rafiki yake ndugu Doane, ambaye hima alighani tuni/vokali ambayo imekuwa ikiimbwa tangu hapo. Kulingana na kura ya maoni ya nyimbo za MUNGU iliyofanyika kipindi fulani huko nyuma kupitia jarida la The Christian Herald, ulikuwa wa 12 katika kura. Kati ya nyimbo zinazopendeka, The Old Rugged Cross ulikuwa wa kwanza. Mmoja kati ya marafiki wa karibu wa Fanny, mke wa mwanzilishi wa the Metropolitan Life Insurance Company, alijulikana kama Mrs. Joseph Knapp. Moja kati ya ziara zake kwa wanawake vipofu katika mwaka wa 1873, alileta muziki alioghani. Mara kwa mara aliupiga kwenye piano. Aliuliza, "Fanny, ni nini tuni hiyo inakueleza?" Akisita kwa muda, alijibu, "Uhakika wa Baraka, Yesu ni wangu!" Moja ya nyimbo kubwa sana za injili ya nyakati zote ilizaliwa.
Part [B] ya makala hii itatuijia kabla ya mwisho wa juma hili, ambapo tutaona jinsi upako wa Fanny ulivyo-influence wahubiri wakubwa wa kimataifa tulionao leo hii.
Pia niwatake radhi kwa kutotimiza ahadi ya kuwaletea makala hii ndani ya juma lililopita kama nilivyoahidi, naona shetani alitaka kumtumia Kaisari anikipu bize.
KWELI MWANAMKE NI KANISA, KWELI MWANAMKE NI JESHI KUBWA.

By Majwala Of Marafiki Huru Forum
Post a Comment

Popular Posts

Blogger templates

Categories

Blog Archive

Google+ Followers

Subscribe Here

Popular Posts